Thursday, June 8, 2017

RC Mghwira asisitiza hajaachia uenyekiti wa ACT

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema hajaachia ngazi yake ya uenyekiti wa Chama cha ACTWazalendo mpaka Juni 15 Kamati Kuu ya chama hicho itakapokaa na kujadiliana kuhusu suala hilo.


Akihojiwa na mwandishi wa habari hizi jana kabla ya kwenda mtamboni kuhusu nafasi yake kwenye chama kukaimiwa na Yeremia Kulwa mpaka Machi mwakani wakati wa uchaguzi mkuu wa chama hicho, Mkuu huyo wa mkoa alisema kwa sasa chama kimemweka kaimu na ni kitu cha kawaida pale mtu mwenye nyadhifa fulani anapokuwa nje ya ofisi.
Alisema, "Sijaacha Uenyekiti, kwa kawaida nikiwa mbali na ofisi au nikiwa nimesafiri, nafasi yangu imekuwa ikikaimiwa ili shughuli za chama ziendelee. "Kwa kuwa nipo Kilimanjaro na nitakuwa na majukumu mengi kwa kipindi hiki, ni sawa nafasi yangu kukaimiwa na mtu mwingine."
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa leo ataanza kazi na shughuli ya kwanza itakuwa ni kufika ofisini na kusaini kitabu cha mahudhurio kisha atafanya kikao na kamati ya ulinzi ya mkoa huo.
Pia alisema atakutana na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wa mkoa huo ili kufahamiana na kujua jinsi atatekeleza ilani ya chama hicho, kisha ataenda kuhani msiba wa Mbunge wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Philemon Ndesamburo aliyezikwa juzi mjini Moshi.
Baada ya kufanya hivyo atarejea ofisini na kuendelea na majukumu mengine yatakayokuwa mezani kwake. Kwa mujibu wa taarifa ya Kaimu Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Samson Mwigamba iliyotolewa jana, Kamati ya Uongozi (kwa mujibu wa Ibara za 29 (24) ya Katiba ya ACT Wazalendo) ilitangaza kumteua Yeremia Maganja kukaimu nafasi hiyo ya Mghwira mpaka uchaguzi mkuu utakapofanyika.

No comments:

Post a Comment